Na Mwandish wetu,Hanang;
BENKI ya Biashara ya Mkombozi imeunga mkono jitihada ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya kiasi cha sh. Milioni 7.7 ikiwa na lengo la la kuwashika mkono waathirika wa maporomoko ya tope kutoka milima ya Hanang yaliyotokea Disemba 3,2023 kwenye mji mdogo wa Katesh.
Miongoni mwa vifaa hivyo walivyovitoa ni pamoja na rangi za nyumba za mafuta na maji,(Primer,Solvent,Red Oxide,Black Paint),roller brush na Hand brush.
Akizungumza hayo juzi Mkoani Manyara wilayani Hanang,Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo, Respige Kimati alisema benki yao ni ya wananchi ipo mbele katika kuhakikisha inatoa huduma mbalimbali za kibenki nchini na katika nyakati kama hizo wamekuwa wakiungana na watanzania kuwashika mkono kama walivyofanya kwa wananchi wa Hanang kwa namna moja ama nyingine kuwarudisha katika hali yao ya kawaida.
Alitoa shukrani kwa serikali kwa ngazi zote kuwa na ushirikiano mkubwa na benki yao katika utoaji wa huduma zao hivyo wanahaidi kuendelea kushikamana na serikali katika shughuli za kuleta maendeleo kwa wananchi.
”Tunafurahi sana siku ya leo kukabidhi vifaa hivi kwa ofisi ya Mkuu wa Wilaya hii ya Hanang kama msaada wetu ili kwa utaratibu mliojiwekea uweze kuwafikia wale wote wananchi waliopata na maafa,”alisema na kuongeza
”Tunatoa pole kwa wale waliopatwa na maafa ambao walipoteza ndugu na jamaa zao,benki ya mkombozi inatazama na kushughulika na wateja wa aina zote,tumeweka kipaumbele kwa wateja wadogo wadogo wakiwemo wa vijijini na kujenga mtandao ambao utaimarisha utoaji wao wa huduma za kibenki,”alisema
Baada ya kupokea msaada huo,Mkuu wa Wilaya ya Hanang, Janeth Mayanja alishukuru uongozi wa benki hiyo kwa kufika katika wilaya hiyo kwa kwenda kuwapa pole waathirika na kuwapatia vifaa vya ujenzi vitakavyosaidia katika shughuli zinazoendelea kufanyika za ujenzi wa nyumba za waathirika hao.
Alisema takribani nyumba 108 zinatarajia kuanza kujengwa ndani ya wiki hii,huku miundombinu mbalimbali ikiwa imekamilika katika eneo hilo la ujenzi ikiwemo Maji,Umeme pamoja na miundombinu ya barabara.
”Tunashukuru Mkombozi Benki kwa kutukimbilia kwa upendo wenu,
Hanang inaendelea kurudi katika hali yake ya awali hatua kwa hatua,hivyo vifaa hivi tulivyopokea lengo lake kubwa ni kuongeza nguvu katika ujenzi huu wa nyumba,”alisema na kuongeza.
“Tunashukuru kwa kutukimbilia na kumuunga mkono Rais Samia kama tunavyojua Rais Samia ameamua kujenga nyumba hizi 108,Shule na kituo cha afya kwaajili ya waathirika hawa hivyo moja ya matumizi yake ya msingi katika ujenzi wa nyumba hizi ili zikamilike ni vifaa hivi mlivyotupatia leo,”alisema.
Aidha aliwasihi uongozi wa benki hiyo kuangalia namna ya kuwagusa wakulima,wafanyabiashara katika kuwainua kiuchumi kwa kupitia benki hiyo.
”Tunafahamu huku hamna tawi hivyo tunawakaribisha kwani kunawatanzania wanahitaji huduma mnazofanya,”alisisitiza.
Maafa hayo yalitokea Jumapili alfajiri Desemba 3,2023 kwenye mji mdogo wa Katesh na Vitongoji vya karibu vya Jorodom,Ganans,Katesh na Dumbeta pamoja na vijiji vya Gendabi na Sarijandu.