Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na Kikosi kazi cha madini Taifa linawashikilia watuhumiwa kumi (10) wote wakazi wa Ilomba Jijini Mbeya kwa tuhuma za kusafirisha, kutorosha vipande vya madini aina ya dhahabu.
Akizungumza na waandishi wa habari Machi 19, 2024 Waziri wa Madini Mhe.Anthony Mavunde amesema watuhumiwa walikamatwa Machi 16, 2024 huko maeneo ya Veta Ikulu, Jijini Mbeya kwenye nyumba ambayo walikuwa wamepanga wakiwa na vipande 314 vya madini aina ya dhahabu vyenye uzito wa gramu 9,622.76 sawa na thamani ya shilingi 1,515,621,987.03 bila kuwa na kibali cha kusafirisha madini hayo.
Aidha, walikutwa na vifaa vingine kama vile Majiko, Gesi, vipimo vya dhahabu pamoja na kasiki ya kuhifadhia fedha.
Watuhumiwa wamekuwa wakitorosha madini hayo kupitia njia zisizo rasmi kwa lengo la kukwepa kulipa Kodi na gharama nyingine zinazohitajika kwa wafanya biashara ya madini.
Naye, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Benjamin Kuzaga (SACP) ametoa wito kwa viongozi wa serikali za Mitaa na Mabalozi kuhakikisha wanahuisha daftari la wakazi ili kubaini wananchi wanaoingia na kutoka katika maeneo yao pamoja na kushirikishana na Polisi Kata waliopo kwenye maeneo yao.
Sambamba na hilo, Kamanda Kuzaga amewataka wafanyabiashara ya madini kufuata taratibu ikiwa ni pamoja na kukata vibali vya kufanya biashara hiyo na kulipa gharama zinazohitajika ili kuepuka usumbufu na hasira pindi wanapobainika kufanya biashara bila kufuata utaratibu.
#KonceptTvUpdates