Kupatikana kwa kutumia ya simu ya mkononi
- Kuongeza uharaka wa upatikanaji wa bima nchini
Katika jitahada za kuleta usawa katika matumizi ya bima nchini, Vodacom Tanzania, kupitia huduma zake za VODABIMA zinazopatikana kupitia M-Pesa, imezindua kampeni kabambe ya Bima Kidijitali ambayo itanufaisha wagonjwa wa kulazwa na kutwa, vyombo vya moto (magari na pikipiki) na bima ya maisha kwa mtu mmoja mmoja na vikundi kwa gharama nafuu.
Akizungumza katika uzinduzi huo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa M-Pesa, Epimack Mbeteni, amesema baada ya kuzindua bima ya vyombo vya moto kwa kushirikiana na washirika 16 nchini, hivi karibuni walizindua Bima ya Afya ya mtu mmoja mmoja kwa kushirikiana na Assemble Insurance na Bima ya Maisha kwa mtu mmoja mmoja kupitia ushikirikiano na Sanlam insurance pamoja na Bima ya Maisha kwa vikundi kwa ushirikiano na Jubilee Insurance katika harakati za kampuni hiyo za kuongoza mapinduzi ya kuleta urahisi wa huduma katika sekta hii nchini kote.
“Tunafuraha kuzindua kampeni hii kabambe ya bima ambayo itajumuisha bima zetu zote kama vile ‘AfyaPass’ ambayo itawezesha wagonjwa wote wa kulazwa na kutwa kupata huduma katika hospitali mbalimbali nchini kote. Huduma hii, ambayo inapatikana kupitia simu ya mkononi kupitia M-Pesa, inalenga kurahisisha upatikanaji na kuongeza wigo wa matumizi ya bima kwa kila mtumiaji. Tumefanikisha hili kutokana na unafuu wa gharama, ambapo gharama za mwaka ni shilingi za Kitanzania 70,000 kwa kila mmoja. Pia, unaweza kumuongeza mtu mwingine wakati wowote, sehemu yoyote kwa sababu kila kitu kinafanyika kupitia simu yako ya mkononi,” anafafanua Mbeteni.
Mkurugenzi huyo aliongezea kwa kutaja bima ya vyombo vya moto ambapo mteja anapata bima zote zikiwemo ndogo na kubwa kwa gharama nafuu. “Pia tuna bima ya maisha ambayo inamhudumia mteja mmoja mmoja pamoja na bima ya maisha kwa vikundi.”
Akiongelea huduma hii, Kamishna wa Bima kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Dk Baghayo Saqware alisema, “kupitia urahisi wa upatikanaji wa huduma za bima nina uhakika kwamba namba ya watumiaji wa huduma za bima itaongezeka zaidi, maana kwa mwaka 2022, watumiaji wa bima walikuwa milioni 17.8 ambayo ni sawa na asilimia 28.9 ya Watanzania wote (61.7m).
Kupitia ubunifu wa kidijitali, VodaBima inalenga kufanikisha njia nafuu ya kupata huduma za bima, ili kupunguza urefu wa muda unaotumika kwa mtu kupata huduma hiyo, na hii itawezekana kwa sababu mteja atatumia simu yake ya mkononi ili kuweza kuwafikia watoa huduma wa VodaBima.
“Uzinduzi huu unaendana na kuunga mkono juhudi za Serikali kuhakikisha Watanzania wote wanapata huduma za bima bila kujali hali yao ya kiuchumi. Kwa kutumia mtandao wetu mpana wa mawasiliano ya simu za mkononi, ambao unawafikia wateja zaidi ya milioni 20 nchi nzima, tunaamini watu wengi watapata faida na kufikiwa kwa njia yenye ufanisi zaidi. Kujiunga na VodaBima ni rahisi na nafuu kwa sababu haitohitaji watu kutembelea ofisi za bima, na wanaweza kulipa kidogo kidogo kulingana na uwezo wao,” aliongeza Mkurugenzi wa M-Pesa.
Tangu kuanzishwa kwake zaidi ya miaka miwili iliyopita, VodaBima imeuza zaidi ya bima milioni 1.5 kwa zaidi ya wateja 200,000 ikiwa ni jumla ya huduma za bima za magari, afya na maisha.
“Napenda kutumia fursa hii kuwasihi wateja wetu na Watanzania kwa ujumla kutumia fursa hii ipasavyo. Huduma hii ni muhimu kwa kila mtu kwa sababu inatuandaa kwa matukio ambayo hatukuyatarajia na kutuondolea wasiwasi tunapokutana na matatizo. Hakuna anayejua ni lini atakumbana na matatizo. Kwa hiyo, suluhisho pekee ni kuwa na bima ya kujilinda wewe na wapendwa wako,” alihitimisha Mbeteni.
-MWISHO-