Upatikanaji wa huduma ya maji katika Wilaya ya Momba, mkoani Songwe unatarajia kutoka asilimia 51 mwaka 2024 hadi asilimia 87 mwaka 2025.
Jumla ya wakazi 133,612 katika vijiji 30 vya wilaya ya Momba sawa na asilimia 51 wanapata huduma ya maji safi na salama kwa kutumia vyanzo vya maji ya mtandao wa mabomba na visima.
Naibu Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) amesema hayo katika hafla ya kukabidhi kisima kwa wananchi wa Kijiji cha Ipumpila ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Wiki ya Maji Kitaifa 2024.
Mhandisi Mahundi amesema kisima hicho kimechimbwa na serikali kwa gharama ya shilingi milioni 41, hii ni pamoja na kuweka miundombinu ya kutoa maji na kwamba katika kipindi cha uongozi wa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, Wilaya ya Momba imetekeleza jumla ya miradi 17 yenye thamani ya shilingi 5,113,433,491 ambayo inayohudumia vijiji 20.
“Miradi hii imeongeza hali ya upatikanaji wa maji katika Jimbo la Momba kwa asilimia 32.53 kutoka asilimia 18.47 mwaka 2020 na kufikia asilimia 51 mwaka 2024” Mhe. Mahundi amesema.
Meneja wa Wakala wa Maji safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya Momba, Mhandisi Beatus Katabazi amesema mradi huo umetekeleza kwa gharama ya shilingi milioni 41.94 na unatarajia kuwanufaisha jumla ya wakazi 2418.
Amesema mradi huo ni miongoni mwa miradi ya ujenzi wa miundombinu midogo ya maji (Point Source 23) inayoendelea kujengwa katika wilaya ya Momba kwa gharama ya shilingi Milioni 285 kati ya shilingi Milioni 500 zilizopelekwa na serikali wilayani humo.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mateo Chikoti, amepongeza jitihada za serikali katika kushughulikia changamoto ya maji katika Wilaya ya Momba ambapo amesema mwaka 2019 kulikuwa na vijiji sita pekee vinavyopata maji, lakini hadi kufikia sasa jumla ya wakazi133,612 wanapata huduma ya maji safi na salama.
#KonceptTvUpdates