Serikali ya Marekani imepanga kuipa Tanzania kiasi cha fedha Tsh: Bilioni 980 kwa mwaka 2024/25 ili kusaidia kutekeleza vipaumbele vya Serikali kupitia Wizara ya Afya katika kupambana na VVU na UKIMWI hapa nchini. Waziri Ummy amesema hayo Machi 25, 2024 wakati wa kikao cha kupitisha bajeti ya PEPFAR kilichofanyika katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya Jijini Dar Es Salaam. “Tunaishukuru sana Serikali ya Marekani kwa kuendelea kuipatia Tanzania msaada kwa zaidi ya miaka 20 kwa ajili ya kupambana na Virusi vya UKIMWI (VVU) na UKIMWI, ambapo kwa sasa watatusaidia Bilioni 980 kwa ajili ya kupambana na ugonjwa huo.” Amesema Waziri Ummy Waziri Ummy amesema Tanzania kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo inaendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuyafikia makundi ambayo bado yana maambukizi mapya kwa kiwango kikubwa kama vile wasichana rika balehe na wanawake vijana (AGYW) pamoja na vijana rika balehe na wanaume vijana (ABYM). Kikao hicho kimehudhuriwa na Balozi wa Marekani Nchini Mhe. Michael Battle na Mtendaji Mkuu wa PEPFAR Duniani Balozi Dkt. John Nkengasong ambapo kwa pamoja wamejadiliana namna ya kuendeleza ushirikiano huo baina ya Tanzania na Marekani katika Sekta ya Afya. Balozi wa Marekani Nchini Tanzania Mhe. Michael Battle ameipongeza Tanzania kwa kuendelea kufanya vizuri katika kufikia malengo ya asilimia 95 tatu.
#KonceptTvUpdates