Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amepokea Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2022/23 kutoka kwa Bw. Charles Kichere Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma tarehe 28 Machi, 2024.
“Kufikia tarehe 30 Juni 2023 deni la serikali lilikuwa shilingi trilioni 82.25 sawa na ongezeko la asilimia 15 kutoka shilingi trilioni 71.31 kwa mwaka 2021/2022. Deni hilo linajumuisha deni la ndani la shilingi trilioni 28.92 na deni la nje la shilingi trilioni 53.32.” – CAG, Charles Kichere
“Nilibaini kuwa mashirika nane ya umma yalikusanya mapato ya shilingi bilioni 23.27 nje ya mfumo wa kielektroniki wa malipo ya serikali kinyume na waraka wa hazina namba tatu wa mwaka 2017.” – CAG, Charles Kichere
“Mwaka wa fedha 2022/23 hasara [ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya-NHIF] ilikuwa shilingi bilioni 156.77 , ikipungua kutoka shilingi bilioni 205.95 kwa mwaka 2021/22. Aidha michango ya wanachama imeongezeka kwa asilimia 14.6 na matumizi yameongezeka kwa asilimia 10.” – CAG, Charles Kichere
“Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania ulisitisha miradi ya miaka ya nyuma yenye thamani ya shilingi bilioni 26.68 katika mwaka wa fedha 2022/23, hii ni kutokana na tathmini ambayo ilionesha kuwa miradi hii haitekelezeki japokuwa tayari imeshalipiwa fedha. Miradi hii ilifutwa kama hasara.” – CAG, Charles Kichere
“Ukaguzi wa ripoti ya kubadilisha mita za umeme za TANESCO kwa mwaka wa fedha 2022/23 ulibaini kuwa mita 108,088 kati ya mita 602,269 zilibadilishwa na TANESCO kabla ya kipindi cha uhai wa matumizi yake kuisha. Katika mita hizo, mita 13,493 zilibadishwa ndani ya mwaka mmoja baada ya kufungwa na mita 94,595 zilikuwa na muda mfupi wa matumizi kati ya mwaka mmoja hadi miaka 15 kinyume na muda unaokubalika wa miaka 20.” – CAG Charles Kichere
“Kwa mwaka wa fedha 2022/23 Kampuni ya Ndege Tanzania ilipata hasara ya TZS bilioni 56.64, sawa na ongezeko la asilimia 61 kutoka hasara ya TZS bilioni 35.24 iliyoripotiwa mwaka uliopita.” – CAG, Charles Kichere
“Kwa mwaka wa fedha 2022/23 Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limepata hasara ya TZS milioni 894. Hasara hii imepungua kwa asilimia 94 kulinganisha na hasara ya TZS bilioni 19.23 mwaka uliopita.” – CAG Charles Kichere
“Kwa mwaka wa fedha 2022/23 Shirika la Reli limepata hasara ya TZS bilioni 100.7. Hasara hiyo imepungua kwa asilimia 47.32 kulinganisha na hasara ya TZS bilioni 190.01 [mwaka 2021/22] .” – CAG Charles Kichere