Nafasi Muhimu ya Takwimu Huria Katika Kudumisha Uhuru wa Vyombo vya Habari na Kuthamini Ushirikiano kati ya Marekani na Tanzania
Na Balozi Michael Battle, 2 Mei 2024
Toka mwaka 1993, kufuatia mapendekezo ya Mkutano Mkuu wa UNESCO, Siku ya Kimataifa ya Uhuru wa Vyombo vya Habari imekuwa ikiadhimishwa kote duniani kila tarehe 3 Mei. Mwaka huu, nimepewa heshima kubwa kushiriki katika maadhimisho rasmi jijini Dodoma nikijumuika pamoja na maafisa wa serikali, wabia wa kimataifa, na viongozi wa asasi za kiraia. Maadhimisho haya yanaangazia nafasi muhimu ya uhuru wa vyombo vya habari katika kukuza demokrasia imara kwa kuwezesha wananchi kufanya maamuzi yatokanayo na wao kuwa na taarifa sahihi na kuzifanya serikali na viongozi wake kuwajibika kwa umma.
Nchini Marekani, tunawathamini sana raia wenye taarifa sahihi na za kutosha kama msingi wa demokrasia. Ni kwa sababu hiyo uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari vimelindwa kikamilifu katika Marekebisho ya Kwanza (First Amendment) ya Katiba ya Marekani.
Kipindi changu kama Balozi wa Marekani nchini Tanzania kimeimarishwa na kuboreshwa sana kwa kushirikiana na waandishi wa habari wa ngazi na aina zote. Raia wanaoandika au kupasha habari (citizen journalists) wakiwa na nafasi ya kipekee ya kuyaona mambo kwa namna tofauti na watu wengine, wanaweza kubadilisha mwelekeo wa taifa, na weledi wa waandishi wa habari waliofunzwa unabaki muhimu kwa kutoa muktadha na mwelekeo sahihi wa mjadala wa kitaifa. Kwa pamoja, kazi yao inaonyesha wazi jinsi vyombo vya habari huria vinavyopambana na ujinga – adui mkubwa kati ya maadui watatu walioainishwa na Mwalimu Julius Nyerere – na hivyo kuijengea uwezo jamii.
Hata hivyo, nguvu ya taarifa hutegemea ubora wa takwimu zinazounda taarifa hiyo. Katika Siku hii ya Kimataifa ya Uhuru wa Vyombo vya Habari, napenda kuangazia kazi bora ya taasisi iitwayo AidData, Taasisi ya utafiti wa takwimu iliyoko katika Chuo cha William & Mary nchini Marekani, ambayo leo imezindua ripoti inayotathmini thamani ya ushirikiano kati ya Marekani na Tanzania kwa watu wa Tanzania.
Marekani inashirikiana kwa kiwango kikubwa na Tanzania, ikiunga mkono na kusaidi miradi mbalimbali kuanzia miradi ya afya na kuwajengea watendaji uwezo (capacity building) hadi miradi ya kuimarisha utawala wa kidemokrasia. Hata hivyo, ili kuelewa vyema thamani ya ushirikiano huo, ni muhimu kuwa na takwimu zinazoweza kupatikana na kutumiwa kwa urahisi.
Dhamira ya AidData ya kuongeza uwazi wa katika utoaji na usimamizi wa fedha za maendeleo ni muhimu sana. Kwa kutoa takwimu za kina na zinazopatikana kwa urahisi kuhusu jinsi na wapi fedha za msaada zinatengwa na kuelekezwa, AidData inawezesha vyombo vya habari na umma kuziwajibisha serikali na taasisi za kimataifa kwa ufanisi. Raia wote wanapaswa kuweza kuzifikia na kuzitumia takwimu huria kama njia ya kupima ufanisi na matokeo ya uwekezaji katika jamii zao.
Ripoti ya AidData inaonyesha kuwa Marekani, kupitia idara na taasisi za kiserikali, mashirika na watu binafsi, inachangia takriban Dola za Kimarekani bilioni 2.8 kila mwaka (Takriban Shilingi za Kitanzania Bilioni 7,140) kwa maendeleo ya Tanzania. Aidha, tumefungua milango yetu kwa Watanzania kuishi, kufanya kazi, na kusoma nchini Marekani. Hali kadhalika, Kila mwaka, Watanzania waishio nchini Marekani (Tanzanian Diaspora) wamekuwa wakichangia dola milioni 96.4 za ziada katika uchumi wa Tanzania kupitia pesa zinazotumwa nchini kutoka Marekani. Kwa miaka 20 iliyopita,ikiwa mfadhili mkubwa zaidi wa miradi ya kudhibiti maambukizi na matibabu ya VVU/UKIMWI, Marekani imezuia vifo vya mapema vya Watanzania wapatao takriban 750,000.
Kwa kupata takwimu huria, AidData imefanya kazi kubwa ya kupima matokeo ya ushirikiano kati ya Marekani na Tanzania kwa Watanzania wote. Takwimu hizi zinatoa simulizi, simulizi ambayo inawawezesha watu wa Tanzania kufanya maamuzi yatokanayo na taarifa sahihi kuhusu jinsi bora ya kushirikiana na mataifa washirika ili kufikia malengo yao ya maendeleo kitaifa. Natumai kila mmoja atachukua muda kusoma ripoti hii na kutathmini yeye mwenyewe jinsi ushirikiano kati ya Marekani na Tanzania unavyogusa maisha yake ya kila siku.
Wakati wa ziara ya Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris mwaka jana, Rais Samia Suluhu Hassan alisema “Tunajitahidi kujenga taifa la kidemokrasia linalozingatia uwazi na kuheshimu utawala wa sheria.” Tunaunga mkono maono haya ya Rais na tutaendelea kufanya kazi kwa bidii pamoja na Watanzania katika serikali na asasi za kiraia ili kuyafanya maono hayo kuwa hali halisi kwa Watanzania wote.
Leo, ninaungana na Wamarekani, Watanzania, na watu kote duniani, tunapotetea uhuru wa vyombo vya habari na kuunga mkono wananchi kupewa taarifa sahihi na toshelevu. Kwani hakuna uhuru katika jamii bila vyombo vya habari huru, na tunailinda haki hiyo adhimu leo na kila siku.