WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amelipongeza Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) kwa mkakati wake wa kukuza watoto kiimani huku wakilijua na kulishika neno la Mungu.
“Pamoja na shughuli ya uinjilishaji, leo nimeshuhudia watoto wadogo wakisema maneno ya Mungu bila kusoma mahali popote na mwingine akiielezea Misingi ya Kanisa la TAG bila kusoma popote. Hii ni kazi kubwa, mnasathili pongezi.”
Ameyasema hayo leo (Jumapili, Julai 14, 2024) wakati akizungumza na viongozi na waumini wa Kanisa la TAG ambako alimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika Maadhimisho ya Miaka 85 yaliyofanyika kwenye uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.
Amesema kanisa hilo linawafanya watu kuwa wamoja, kuwa na uhusiano wa kiimani na kijamii na kutoa mafundisho ya umuhimu wa kushiriki katika huduma kutoa misaada, elimu, huduma za afya na maendeleo ya jamii.
“Kanisa hili ni mfano katika kukuza umoja na ushirikiano kati ya Wakristo wa madhehebu mbalimbali na waamini wa dini nyingine nchini, kitendo ambacho kinatuwezesha kama jamii kuwa na mshikamano na kuimarisha amani na usalama.
Waziri Mkuu amesema Serikali ina kila sababu ya kuwashukuru Wachungaji na Maaskofu kwa kazi yao kubwa ambayo inaimarisha amani, utulivu na maendeleo katika nchi.
“Serikali inathamini mchango wa taasisi za dini katika kuimarisha maadili mema, kukemea maovu na mmomonyoko wa maadili. Wakati wote Serikali imekuwa ikifanya kazi kwa pamoja na taasisi za dini hususani katika kampeni za kijamii za kuelimisha na kuhamasisha maadili mema na mwenendo mwema kwa wanajamii.”
#KonceptTvUpdates