Naibu katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na utalii anayeshughulikia utalii -Nkoba Mabula ameielekeza Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) kuendelea kubuni mazao mapya ya utalii ili kuwavutia watalii wengi zaidi wanaotembeela nchi yetu.
Mabula ametoa maelekezo hayo baada ya kupokea wasilisho kuhusu hali ya utalii katika hifadhi ya Ngorongoro, uboreshaji wa huduma za utalii, utangazaji wa vivutio vya utalii, mipango ya kubuni na kuendeleza mazao mapya ya utalii pamoja na kuyatangaza kwenye mataifa mbalimbali.
Akiwa katika kikao na menejimenti ya NCAA Mabula amepokea wasilisho la hali ya Utalii katika eneo hilo na mazao mapya ya utalii ambayo yapo kwenye utaratibu wa kutangazwa hivi karibuni ambayo ni Utalii wa baiskeli katika eneo la Olduvai, Utalii wa boti (canoeing) katika kreta ya Empakaai, utalii wa usiku (Night game drive) na utalii wa kuruka Kamba (Zipline tourism).
“Nimeona mikakati ya kuzindua mazao mapya ya Utalii kama utalii wa baiskeli, Zipline, utalii wa boti, endeleeni kuyafanyia utafiti wa kina na muongeze mazao mapya zaidi na yatangazwe katika fursa zenye majukwaa ya kimataifa ili kuendelea kuvutia wageni wengi wanaotembelea nchi yetu” amesisitiza Mabula.
Katika ziara hiyo mabula amekagua pia uboreshaji wa miundomnibu katika barabara kuu ya kutoka lango la Loduare hadi geti la Nabi, barabara ya kushuka bonde la Kreta, vyoo katika bonde la Ngorongoro, mifumo ya Tehama inayotumika katika malipo na kambi maalum za kulala wageni (Campsite).
Ameongeza kuwa “Tuendelee kuboresha miundombinu ya vivutio vingine ambavyo havijafikika ili kuongeza uzoefu wa maeneo mengine kwa wageni wetu tofauti na Wanyama ambao wameshazoeleka. Tayari Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonyesha njia kwa Filamu ya Tanzanzia the Royal tour na idadi ya wageni imeanza kuongezeka, tuendeleze zaidi ili kufikia idadi ya watalii milioni 5 kama ilani ya chama tawala inavyotuelekeza” ameongeza Mabula
Naibu Kamishna wa Uhifadhi NCAA (Uhifadhi, utalii na Maendeleo ya Jamii) Vicktoria Shayo ameeleza kuwa NCAA inaendelea kuboresha huduma utalii na kujitangaza katika majukwaa mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa kushirikiana na wadau wa Utalii hali iliyowezesha eneo la hifadhi ya Ngorongoro pekee katika mwaka wa fedha 2023/2024 lilipokea wageni Watalii ni 908,627 ambapo Watalii wa ndani walikuwa 354,752 na watalii wa nje 553,875.
Kwa upande wake Kamishna Msaidizi Mwandamizi huduma za Utalii NCAA Mariam Kobelo amesema ili kuboresha huduma kwa wateja mamlaka hiyo inaendelea kuboresha miundombinu ya Tehama, mafunzo ya huduma kwa wateja na ukaribu kwa wageni na kuweka miundombinu rafiki katika mageti yanayoingiza wageni hifadhini ili wakifika maeneo hayo waatumie muda mfupi wa kupata huduma kwa ajili ya kuendelea na shughuli za utalii kwa wageni.
M:Kassim Nyaki, Ngorongoro.
#KonceptTvUpdates