Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeunga mkono agenda za Shirika la Utalii Duniani (UN Tourism) kuhusu uwekezaji wa kimkakati katika rasilimali watu kwenye elimu na ujuzi pamoja na agenda ya usalama wa maeneo ya utalii lengo likiwa ni kuibadilisha Afrika kwa siku zijazo kupitia ujuzi wa elimu na uwekezaji wa kimkakati katika utalii kwa ukuaji endelevu na shirikishi.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. @AngellahKairuki (Mb) alipokuwa akichangia mjadala wa agenda hizo kwenye mkutano wa 67 wa Mawaziri wa Utalii wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UN Tourism) Kanda ya Afrika (67 CAF) unaoendelea kwenye hoteli ya Radisson Blue jijini Livingstone Zambia.
Amefafanua kuwa kupitia Chuo cha Taifa cha Utalii nchini Tanzania ambacho kipo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kimewekeza katika kuwajengea uwezo wakufunzi na kushirikiana na taasisi nyingine za kimataifa katika utoaji wa mafunzo kwa kubadilishana uzoefu lakini pia kuboresha matumizi ya teknolojia ili kufikia malengo.
Pia, ameongeza kuwa Serikali ya Tanzania inashirikiana na sekta binafsi hasa katika kutambua ombwe la ujuzi katika sekta ya utalii na kutoa mafunzo yanayohitajika ili kukidhi mahitaji ya sekta nzima ya utalii nchini Tanzania.
Aidha, Waziri Kairuki amepongeza juhudi za Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani kwa kuzindua mitaala ya Elimu ya Utalii ya Umoja wa Mataifa na kuweka bayana kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia kuanzishwa kwa mitaala ya utalii.
“Tutaanza na shule za sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne, kisha kidato cha tano na sita kuanzia mwezi Julai mwaka 2025. Sasa tunaandaa mitaala na tutaenda mbali zaidi hasa kwa Shule za mkondo wa Amali” amesisitiza Mhe. Kairuki na kuliomba Shirika la Utalii Duniani kutoa ushirikiano wakati wa utayarishaji wa mitaala ili kupata uzoefu wa wale ambao tayari wameshafanya hivyo.
Kwa upande wa agenda ya uwekezaji wa kimkakati Mhe. Kairuki amefafanua kuwa Tanzania ina Kituo cha Uwekezaji ambacho kimeweka madawati ya uwekezaji hususani katika utalii kwenye mikoa mbalimbali na hivi karibuni kilizindua moja ya kituo katika jiji la Arusha ambalo ni moja ya mikoa ya kitalii nchini Tanzania.
“Tunaendelea kuweka madawati ya uwekezaji katika vituo vyetu vya uwekezaji vya Tanzania na pia kuhakikisha kuwa tunaweka vivutio vya uwekezaji wa utalii ili tuweze kuwa na utalii uendelevu na kukuza uwekezaji katika sekta ya utalii.
Amesema katika taarifa ya uwekezaji ambao umefanyika katika nchi mbalimbali duniani Tanzania imepokea wawekezaji zaidi ya kampuni 12 ambao ni kiwango kikubwa nakuifanya iweze kuingia katika nchi tano bora Barani Afrika ambazo zimeweza kupokea uwekezaji mkubwa katika sekta ya utalii.
Kuhusu Usalama wa maeneo ya utalii, Mhe. Kairuki ameweka bayana kuwa Tanzania inatumia Jeshi la Polisi na imeanzisha vitengo maalum vya kidiplomasia vinavyoshughulikia masuala ya usalama katika sekta ya utalii ikiwemo usalama wa watalii lakini pia mali zao.
“Serikali ya Tanzania pia imekuwa ikitoa ujuzi maalum kwa polisi wa kidiplomasia ili kutumia lakini pia kuboresha huduma kwa wateja wakati wanafanya kazi zao” amesema.
Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Wakala wa Usafirishaji Watalii Tanzania (TATO), Wilbard Chambulo amesema lengo la kushiriki mkutano huo ni kutafuta fursa za kupata wawekezaji kwa ajili ya Sekta ya Utalii nchini Tanzania.
Mkutano huo umehudhuriwa na nchi wanachama wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani, wataalamu katika Sekta ya Utalii, wawakilishi wa taasisi za fedha na huduma za kifedha na wadau kutoka sekta ya umma na binafsi wanaosimamia na kuendeleza mabadiliko chanya katika Sekta ya Utalii Barani Afrika.
#KonceptTvUpdates