Meli kubwa iliyobeba mizigo ya tani elfu 14 imetia nanga katika bandari ya Tanga kutoka nchini China kwa mara ya kwanza baada ya uboreshwaji mkubwa wa bandari hiyo uliogarimu zaidi ya shilingi bilioni 429.
Meli hiyo ya kampuni ya Seefront Shipping Service Ltd, imebeba magari 500 ya mizigo ambayo yanasafirishwa kwenda nchi za DRC Congo, Zambia, Burundi na Rwanda unatarajiwa kukaa bandarini hapo kwa muda wa siku tatu na kuondoka.
Akizungumza wakati meli hiyo ikitia nanga Jijini Tanga,Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile amesema fedha zilizowekezwa katika maboresho hayo zimeanza kuonesha mafanikio kwani utendaji kazi katika bandari hiyo umeongezeka kwa tija.
“Shughuli hii ya leo ni matokeo ya uwekezaji mkubwa wa maboresho yaliyofanyika katika bandari ya tanga , shehena zimeongezeka mara dufu kutoka shehena 470 mwaka 2019 na kufikia milioni 1 ya sasa, pia meli zimeongezeka kutoka 118 2019 hadi 307 mwaka huu,
“Haya ni mapinduzi makubwa yanayoonesha kwamba fedha zilizowekezwa zinaleta tija , amesema Naibu Waziri huyo
kwa upande wa makasha na abiria wameongezeka hata mzunguuko wa fedha kwa Mkoa umeongezeka, hivyo kukamilisha kauli mbiu ya Mkoa huo kwamba ‘Tanga lango kuu la uchumi Afrika’.
Kihenzile alitoa rai kwa Mamlaka ya Bandari nchini kuendelea kuisimamia bandari ya Tanga kwa weledi lakini pia kwa wadau kuchangamkia fursa za kusafirisha abiria kutoka bandarini hapo kwenda visiwa vya Pemba.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi, Dkt. Batilda Buriani amesema Mkoa upo kimkakati ambao una uwezo kibiashara na maboresho hayo yatapunguza wigo wa wafanyabiashara kurundika mizigo bandari ya Dar es salaam kwa kuipitishia Tanga.
#KonceptTvUpdates