Jeshi la Polisi Kamisheni ya Zanzibar limekanusha taarifa za Kutekwa kwa watoto na pia linamshikilia HABIBU RASHID OMAR (35) mkazi wa Mwera ambaye anatuhumiwa kuchapisha taarifa ya uongo kupitia mitandao ya kijamii kuhusiana na kutekwa kwa watoto wanne katika Skuli ya Regezamwendo, hali ambayo imesababisha taharuki kwa jamii.
Akizungumza na waandishi wa habari, Makao Makuu ya Polisi Zanzibar Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Naibu Kamishna wa Polisi DCP ZUBERI CHEMBERA amesema kuwa, Zanzibar ni salama na hakuna tukio lolote la utekwaji wa watoto na kwamba amewataka wananchi kuzipuuza taarifa za upotoshaji zinazosambazwa kupitia mitandao ya kijamii.
“Niwahakikishie kwamba Zanzibar ni salama, watoto wetu wako salama, wanakwenda shule na kurudi nyumbani salama, wazazi tuendelee kuwaangalia watoto wetu, tuendelee kuwatunza watoto wetu kwa maadili mema kama tuna mashaka ya jambo lolote tulitolee taarifa kwenye vyombo vya usalama vinavohusika badala ya kuandika kwenye mitandao ya kijamii ambayo mwisho wake inasababisha taharuki” alisisitiza Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai DCP Chembera.
Aidha, DCP CHEMBERA amesema Jeshi la Polisi linaendelea kufanya uchunguzi na linatarajia kuwafikisha Mahakamani watuhumiwa wote watakaobainika kuhusika na usambazaji wa taarifa za uzushi na upotoshaji.