NA MWANDISHI WETU
MSIMU wa Nne wa Kampeni ya Weka Akiba na Ushinde ulioendeshwa na Benki ya NMB ‘NMB Bonge la Mpango – Mchongo Nd’o Huu,’ umefikia tamati Alhamisi ya Desemba 19, ambako Dennis Theornest Rwegasira wa Kariakoo Dar es Salaam, aliibuka mshindi wa jumla wa kitita cha Sh. Mil. 100.
Bonge la Mpango ilizinduliwa Septemba 25, 2024 na Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Toba Nguvila na Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi na Biashara wa NMB, Filbert Mponzi, ambapo kwa wiki 12, zilichezeshwa droo za kila wiki, kila mwezi na fainali kusaka washindi wa pesa na bidhaa zenye thamani ya zaidi ya Sh. Mil. 150.
Droo ya fainali imeendeshwa kupitia Kipindi cha XXL cha Clouds FM, ikiendeshwa na Mponzi, mbele ya Mkuu wa Mauzo na Mtandao wa Matawi ya NMB, Doantus Richard na wakuu wengine wa idara mbalimbali za Benki ya NMB, wakisimamiwa na Afisa wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania, Lucy Katamba.
Katika droo hiyo, Rwegasira ambaye kitaaluma ni Daktari, alipigiwa simu na kupokea akiwa safarini, ambako licha ya kutoamini ushindi wake, alikiri kuwa yeye ni mteja mtiifu, mwaminifu na wa muda mrefu, huku akiwataka Watanzania kuitumia benki hiyo katika huduma zao, akiitaja kama benki yenye manufaa mengi.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mponzi alisema Bonge la Mpango ni njia moja wapo inayotumiwa na Benki ya NMB katika kurejesha sehemu ya faida yake kwa jamii, ndio maana wakabuni wazo la kuja na kampeni hiyo inayolenga kuhamasisha Watanzania kudumisha utamaduni chanya wa kufungua akaunti na uwekaji akiba.
“Tunapofunga kampeni hii, sio mwisho wa kampeni zenye manufaa kwa Watanzania, ipo NMB MastaBata inaendelea, lakini pia mwaka mpya utaambatana na huduma nyingi muhimu na nzuri kwa wateja wetu ndio maana tunawawasisitiza kila mmoja kuhakikisha anafungua akaunti NMB.
“Wakati tukiwahakikishia wateja wa NMB muendelezo bora wa huduma bora na rafiki kwao, sisi tunaamini kwamba kila Mtanzania anapaswa kuwa na akaunti NMB, Benki Bora kwa miaka 11 mfululizo katika miaka 12 iliyopita,” alisema Mponzi huku akiinadi Akaunti ya Wekeza yenye riba hadi asilimia 12 kwa mwaka.
Ukiondoa Sh. Mil. 100, katika fainali hiyo walitafutwa washindi saba wa pikipiki ya mizigo ya matairi matatu (moja kwa kila mmoja), mshindi mmoja wa trekta ya kilimo ‘power tiller,’ huku washindi wengine wanne kila mmoja akijinyakulia kitita cha Sh. Mil. 5.
Kupitia kampeni hiyo, washindi 10 wa kila wiki walijishindia fedha taslimu Sh. 100,000 kila mmoja, huku washindi wengine tisa wakijinyakulia kimoja kati ya Friji, Televisheni ya kisasa, mashine ya kufulia na jiko la gesi, kulingana na matakwa ya mteja.
Katika zawadi za droo za kila mwezi, benki hiyo ilikuwa ikiwazawadia washindi wanne wa kila mwisho wa mwezi Sh. Mil. 5 kila mmoja, ikiwa na maana wateja wanane katika miezi miwili ya ya NMB Bonge la Mpango, waliojizolea Sh. Mil. 40 kwa wote (wakiwemo wanne waliopatikana kwenye fainali).
NMB Bonge la Mpango ilianza mwaka 2021, kabla ya mwaka uliofuata (2022) kurejea tena kwa kampeni hiyo ikitumia kaulimbiu ya ‘2merudi Tena,’ kisha mwaka jana 2023 kuitwa NMB Bonge la Mpango ‘Moto Ule Ule’ na mwaka huu kuwa NMB Bonge la Mpango ‘Mchongo Nd’o Huu.’
Mwisho