Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), limeahidi kuisaidia Tanzania kwenye masuala ya Lishe ili kukabiliana na Udumavu wa watoto ambao unaathari katika ukuaji wa ubongo na uchumi.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), alipokutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkazi mpya wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) nchini Tanzania, Bi. Elke Wisch, jijini Dodoma.
Mhe. Chande, alisema kuwa Shirika hilo limekuwa likiisaidia Tanzania katika masuala mbalimbali ya kibajeti ambapo katika mwaka wa fedha 2023/ 2024, lilitoa dola za Marekani milioni 20.3 sawa na zaidi ya shilingi bilioni 50 za Tanzania.
Mhe. Chande ameliomba Shirika la Umoja wa Mataifa linalohudumia Watoto (UNICEF ), kuendelea kuiunga mkono Tanzania katika juhudi zake inazozifanya kuboresha maisha ya wananchi wake na kujikwamua kiuchumi.
Aidha amelishukuru Shirika hilo kwa kuendelea kushirikiana na Serikali na aliahidi kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na Shirika hilo wakati likitimiza kazi zake nchini.
Kwa upande wake Mwakilishi Mkazi mpya wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Bi. Elke Wisch, alisema UNICEF inaahidi kuwekeza kwenye lishe ya Watoto ili kusaidia kuondoa udumavu kwa kuwa udumavu unaathari katika ukuaji wa ubongo wa mtoto na pia kupunguza kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi.
Alisema kuwa Shirika lake linajitahidi kuhakikisha linasaidia masuala ya kibajeti na program zinazoendelea nchini Tanzania kwa kuwa lengo lao ni kusaidia katika maendeleo ya watoto na wanawake kama nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa, na UNICEF kama Wakala wake.
Bi. Wisch alisema kuwa amekuja kujitambulisha lakini pia kuelezea maeneo ambayo watawekeza kwa kushirikiana na Tanzania ikiwa ni pamoja na kuwawezesha watoto pamoja na sekta za fedha.
Aidha aliipongeza Tanzania kwa ushirikiano inaouonesha kwa Shirika hilo na hivyo kusaidia kuchochea maendeleo katika suala la lishe ya watoto na wanawake lakini pia suala la elimu, mabadiliko ya tabianchi na maendeleo endelevu.
#KonceptTvUpdates