Jana wakimbizi kutoka katika kambi za Nyarugusu na Nduta zilizopo mkoani Kigoma waliungana na watu wengine ulimwenguni kuadhimisha siku ya maji duniani ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni maji safi kwa maendeleo endelevu.
Maadhimisho hayo yaliandaliwa kwa ushirikiano kati ya serikali kupitia idara ya wakimbizi na mashirika mbalimbali yanayotoa misaada katika makambi hayo yakiwemo UNHCR, UNICEF, International Rescue Committee, Oxfam, TWESA, Save the Children, Water Mission, TCRS na mengine mengi.
Maadhimisho hayo yalipambwa na burudani mbalimbali zikiwemo ngoma na maigizo na kisha risala zilizosisitiza umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji.
Kwa mujibu wa shirika la kuhudumia wakimbizi UNHCR hadi sasa kuna wakimbizi kutoka mataifa mbalimbali zaidi ya 140,000 wanaoishi katika kambi ya Nyarugusu huku katika kambi ya Nduta kuna wakimbizi takribani 50,000 kutoka Burundi.
Tangu kufunguliwa tena kwa makambi hayo mwaka jana, mashirika mbalimbali yamekuwa yakitoa misaada ya kibinadamu katika makambi likiwemo shirika la Oxfam ambalo linatoa huduma za maji na ujenzi wa vyoo ikiwa ni pamoja na kuwafundisha wakimbizi namna mbalimbali za kuishi kwa kuzingatia kanuni bora za afya ili kujilinda dhidi ya magonjwa.