Benki ya Exim imeandaa futari ya pamoja kwa wateja wake katika hafla iliyofanyika katika hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam mnamo tarehe 15 mwezi Machi 2024.
Mgeni Rasmi katika tukio hili alikuwa Sheikh Mkuu wa Mkoa Dar es Salaam, Sheikh Walid Alhad Omar, akiwakilisha waumini wa dini ya Kiislam ambao wapo kwenye mfungo katika mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani.
Akizungumza katika hafla hiyo, Sheikh mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, Sheikh Walid Alhad Omar, aliipongeza Benki ya Exim kwa juhudi zake katika kukuza maendeleo ya kijamii na kueleza shukrani zake kwa mchango wa benki hiyo kwa jamii. Alisema, “Benki ya Exim inaonyesha dhamira ya kweli katika kutumikia wateja wake na jamii kwa ujumla, lengo kuu la Ramadhani ni kuleta watu pamoja, na usiku huu, benki ya Exim imehakikisha kuendeleza lengo hilo kwa vitendo”.
Bwana Jaffari Matundu, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Exim, aliwakaribisha wadau wote katika Iftar hiyo huku akitambua mahusiano mazuri ya tija yaliopo baina ya Benki ya Exim na wateja wake na umuhimu wa kuyaendeleza kwa ajli ya ustawi na maendeleo ya jamii.
“Wateja wetu ni zaidi ya wateja tu, ni sehemu muhimu ya familia yetu. Tunaona kila mmoja wenu kama mshirika na mwenzetu katika safari yetu ya mafanikio”, alisisitiza Jaffari Matundu.
Pia, Mkurugenzi huyo alizungumzia hatua na maboresho mbalimbali ambayo yamefanywa na benki ya Exim ili kuendana na mabadiliko katika sekta mbalimbali ikiwemo maendeleo ya teknolojia ya kidijitali na kusogeza huduma kwa wateja.
Jaffari alifafanua kuwa, “tumefanya maboresho makubwa katika mfumo wetu wa Benki ili kuendelea kuhudumia wateja wetu vizuri zaidi kwa kutoa huduma zinazoendana na mabadiliko ya kidigitali”.
“Vile vile tumeendelea kuongeza idadi ya Mawakala wetu (maarufu kama Exim Wakala) ili kuleta huduma zetu karibu na wateja wetu popote walipo”, alimalizia Afisa Mtendaji Mkuu huyo.
Exim Bank pia imeboresha huduma za kidijitali kwa wateja wake ambapo wanaweza kupata huduma za kibenki popote pale walipo ndani na nje ya Tanzania. Hii ni kwa lengo la kurahisisha upatikanaji wa huduma za kibenki kwa wateja wao na maendeleo ya teknolojia yanayoendelea kutokea duniani.