Aliyewahi kuwa Mbunge wa Arusha Mjini (CHADEMA), Godbless Lema, ameshauri kuwa kasi ya kusaka ‘maokoto’, iende sambamba na wajibu wa kuandaa watoto ili wawe raia wema kesho.
Lema ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Kanda ya Kaskazini, ametoa ushauri huo kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.
“Kama una uwezo wa kumfanya mke wako Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa familia yako tu na kumlipa ni muhimu sana kufanya hivyo. Majukumu yake yawe kufundisha watoto utu, maadili, nia njema na kumcha Mungu,” ameandika Lema.
Ameongeza: “Jamii ya sasa ina outsource sana malezi, ni hatari sana katika ulimwengu huu wa utandawazi. Tunakimbizana na pesa ili tulee watoto halafu watoto wanakosa muda wa malezi kutoka kwa wazazi wao, mwalimu wao anakuwa internet na televisheni. Tutakuwa na jamii ngumu sana katika siku za usoni.”