#USALAMA Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania limefanikiwa kumkamata mtu mmoja aitwaye Samwel Mbise (42) mkazi wa Sanawari Jijini Arusha akiwa anafanya biashara ya kubadilisha fedha za kigeni bila ya kuwa na kibali.
Akitoa taarifa hiyo leo Julai 31, 2024 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Justine Masejo amebainisha kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa kupitia operesheni ambayo inaendelea iliyoanza Julai 29, 2024 ambapo alikutwa na fedha mbalimbali.
SACP Masejo amefafanua kuwa mtuhumiwa huyo alikutwa na fedha mbalimbali ambazo ni Dola za Marekani 5,952, Euro 835, Dola za Canada 1,845, Pound 45, Switzerland Franc 20, Dola za Australia 50, Qatar Riyals 05, Pound za Egypt 25, Shilingi za Kenya 38,400/= na Shilingi za Tanzania 52,552,000/= ambazo jumla yake ni fedha za Kitanzania 75,809,649/=.
Aidha Jeshi hilo linaendelea kumhoji mtuhumiwa huyo na pindi upelelezi utakapokamilika jalada litapelekwa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka kwa hatua zaidi za kisheria.
Sambamba na hilo Jeshi la Polisi mkoani humo linawataka baadhi ya watu wanaojihusisha na biashara za kubadilisha fedha za kigeni kuhakikisha wanafuata taratibu za kisheria kama miongozo ya Benki Kuu ya Tanzania inavyoelekeza ili kuepuka mkono wa sheria.
#KonceptTvUpdates