Mshambuliaji wa klabu wa Manchester City, Erling Haaland, kwa mara nyingine tena ameteuliwa kuwania tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwaka katika Tuzo za Chama Cha Wachezaji wa Kulipwa nchini England (PFA).
Haaland anawania tuzo hiyo pamoja na wachezaji wenzake wa Manchester City, Phil Foden na Rodri ambapo ameteuliwa kuwania kwa mara ya pili.
Haaland ameteuliwa kwenye orodha ya wachezaji sita kwa upande wa Wanaume baada ya kufunga mabao 27 msimu uliopita na kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya England
Aidha, Haaland, alionyesha mchezo bora kwa kufunga magoli 38 katika mechi zote, huku City ikinyakua taji la Ligi Kuu ya England kwa msimu wa nne mfululizo.
Nyota huyo raia wa Norway alishinda Tuzo ya Mchezaji Bora wa kulipwa, hatua inayokuja baada ya klabu yake kuonyesha mchezo wa viwango vya juu katika msimu wa 2022/23.
Kwa upande wake Rodri, alikuwa kiungo muhimu katika kikosi cha City wakati wa ushindi wao wa Ligi Kuu ya England na pia alisaidia timu ya Taifa ya Spain kushinda Euro 2024.
Mchezaji wa England, Foden, alifunga magoli 27 msimu uliopita akiwa na kikosi cha Manchester City.
Mshambuliaji wa Chelsea, Cole Palmer, kiungo wa Arsenal, Martin Odegaard, na mshambuliaji wa Aston Villa, Ollie Watkins, pia wameteuliwa kuwania tuzo hii.
Washindi watajulikana katika hafla ya tuzo za PFA itakayofanyika mjini Manchester mnamo Agosti 20, 2024.