Gazeti la Dira ya Mtanzania, Toleo Na.404 la Februari, 29 – Machi 6, 2016 liliandika taarifa yenye kichwa cha habari kisemacho “Uchafu wa Ombeni Sefue Ikulu”. Taarifa hiyo, ambayo ni muendelezo wa makala nyingine kwenye toleo la gazeti hilo la wiki iliyopita, ilimtuhumu Katibu Mkuu Kiongozi kushawishi juu ya uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa MSD pamoja na Kampuni za “CRJE” na “UGG” kupewa tenda ya kujenga Chuo Kikuu cha Dodoma, Daraja la Kigamboni na Reli ya Dar es Salaam – Kigali. Taarifa zote hizi ni za uongo na za kupotosha wananchi.
2. Kuhusu uteuzi wa nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa MSD,
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, hakuhusika kwa namna yoyote kushawishi uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa MSD.
Uteuzi huo ulitekelezwa kwa kufuata kanuni na taratibu zilizowekwa. Nafasi hiyo ilitangazwa na Bodi tarehe 20 Novemba, 2013.
Usaili ulifanywa na kampuni huru iliyopewa jukumu hilo na Bodi. Mapendekezo ya majina matatu yalipelekwa kwa Mhe. Rais na Waziri wa Afya, kwa ajili ya uteuzi.
Balozi Sefue alikuwa hamjui aliyeteuliwa na wala hakuwahi kuwa na uhusiano naye. Alichofanya Balozi Sefue ni kutangaza tu uteuzi baada ya Rais kuteua.
Gazeti hilo pia limeandika uwongo kuwa MSD haijawahi kuongozwa na Mkurugenzi Mkuu asiye Mfamasia.
Tangu MSD ianzishwe mwaka 1993 hadi sasa, ni Mkurugenzi Mkuu mmoja tu, Rino Meyers (1996-1999), ndiye alikuwa Mfamasia. Wakurugenzi wengine kama Peter Mellon (1993-1995), Jay Drosin (2001-2004) na Joseph Mgaya (2004-2013) hawakuwa Wafamasia.
3. Kuhusu Kampuni ya CRJE kuhusishwa na Balozi Ombeni Y. Sefue
Suala la kumhusisha Katibu Mkuu Kiongozi na kampuni hii nalo ni uzushi na uongo wa kupindukia.
Wakati kampuni hii ikipewa tenda ya kujenga Chuo Kikuu cha Dodoma mwezi Oktoba 2007, Balozi Ombeni Y. Sefue hakuwa Katibu Mkuu Kiongozi; alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Marekani.
Kadhalika mchakato wa kumpata mkandarasi wa daraja la Kigamboni, ulipoanza mwezi Machi, 2011, Balozi Sefue hakuwa Katibu Mkuu Kiongozi; alikuwa Balozi wa Tanzania, Umoja wa Mataifa, New York.
Hata mkataba wa ujenzi wa Daraja hilo uliposainiwa tarehe 9 Januari, 2012, Balozi Sefue alikuwa na wiki moja tu ya kuwa Katibu Mkuu Kiongozi kufuatia kuteuliwa tarehe 30 Disemba, 2011.
Aidha, Kampuni iliyoshinda tenda hiyo wala siyo CRJE kama ilivyoandikwa na gazeti hilo bali ni China Major Bridges Engineering Company (BCEC) kwa kushirikiana na Kampuni ya China Railway Construction (CRCEG).
4. Kuhusu tuhuma kuwa Katibu Mkuu Kiongozi kuipigia Chapuo Kampuni ya UGG:
Katibu Mkuu Kiongozi hajawahi kuipigia chapuo kampuni yoyote ile pahala popote. Isitoshe, hakuna kampuni yenye jina la “UGG” iliyowahi kuonesha nia ya kujenga reli ya kati.
Hii ni moja ya uthibitisho kwamba gazeti hili linatoa taarifa za kuokoteza zisizo na ukweli kama vile walivyopotosha kuhusu jina la Katibu Mkuu Kiongozi kwenye makala yao ya pili kwenye ukurasa wa tisa wa gazeti hilo yenye kichwa cha habari “Magufuli anaishi na jipu Ikulu” ambapo walimpachika Katibu Mkuu Kiongozi jina la Sifuni, jina ambalo hajawahi kuwa nalo.
Balozi Sefue hajahusika, hahusiki na wala hatahusika katika kuchagua wa kupewa tenda hiyo kwa sababu yeye si sehemu ya wenye mamlaka ya kutoa tenda.
5. Kuhusu Eliachim Maswi:
Gazeti la Dira ya Mtanzania limeandika kuwa moja ya “madudu” aliyofanya Balozi Sefue ni walichoita kumsafisha Bwana Eliachim Maswi.
Wanadai hivyo wakati wamekiri kuwa alichofanya Balozi Sefue ni kusoma matokeo ya uchunguzi, ambao hakuufanya yeye.
Waliomsafisha Maswi ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali; Sekretarieti ya Maadili ya Umma; na hatimaye kamati ya uchunguzi iliyoongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu. Kwa hiyo, kwa maoni ya gazeti hili, Balozi Sefue asingepaswa kusoma matokeo ya uchunguzi
uliofanywa na vyombo hivyo huru. Kwa maoni yao kusoma taarifa ya
uchunguzi ni “madudu”.
6. Hitimisho:
Kwa kuwa habari hizo hazina chembe yoyote ya ukweli, na wao wenyewe ndani ya gazeti wamekiri hawana ushahidi, ni wazi kuwa habari hizo ni za kubuni na zimetungwa.
Kwa sababu hiyo, Serikali inalitaka Gazeti la Dira ya Mtanzania kukanusha uongo na uzushi wao na kumuomba radhi Balozi Ombeni Sefue, kuiomba radhi Serikali na kuwaomba radhi wote walioumizwa na uzushi huo kwa uzito ule ule uliotumika kuchapisha taarifa hiyo.
Vinginevyo iwapo gazeti la Dira ya Mtanzania lina ushahidi wa huo “uchafu” wa Katibu Mkuu Kiongozi, waupeleke mara moja kwenye vyombo vinavyohusika ikiwamo Sekretarieti ya Maadili na TAKUKURU.
Vinginevyo, hatua zikichukuliwa dhidi yao wasiseme Serikali inavibana vyombo vya habari.
Aidha Serikali inashauri wenye vyombo vya habari, wachapishaji, wahariri na waandishi wa habari wajikite kwenye weledi na ukweli, wafanye utafiti na kuandika mambo waliyo na uhakika nayo, na kamwe wasikubali kutumiwa kuendeleza agenda za watu wengine.
Imetolewa na Idara ya Habari – MAELEZO.
01 Machi, 2016