Na Mwandishi Wetu; Timu ya kuwakilisha Wananchi kutoka Visiwani Zanzibar imesafiri mpaka Ikulu jijini Dodoma kwa kutumia Vespa (Honda) kwenda kumpa maua Rais wa Jamuhuri ya Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kusherehekea nae katika Sikukuu ya wapendanao.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Februari, 12, 2024, Kiongozi wa Msafara huo wa timu iliyochaguliwa kutoka Zanzibar kwa ajili ya kupeleka maua kwa Rais Tanzania Bara, Salum Stika amesema wameona vizuri kusherehekea siku hiyo wakiwa pamoja na Mama.
“Sisi kutoka Zanzibar tumeridhia na tumependezwa na uongozi wa Mh Rais na tumeungana na Wtanzania wenzetu kutoka Butiama, Arusha na maeneo mengineyo kumpa mama yetu maua yake msimu huu wa siku ya wapendanao,” amesema Stika.
Pia wamefunguka kuwa wameamua kutumia usafiri huo ili kuonyesha utamaduni wao kwa sababu Vespa ndio utamaduni wao.
Mmoja wa madereva ambao wanaendesha vespa Khadija Saleh amesema kutokana na kazi kubwa anayoifanya Rais ameona ni vyema kuungana na wenzao ili kuweza kwenda kumpongeza.
“Sisi Wazanzibar tumeona kazi kubwa ambayo mama anaifanya anathamini sana jinsia katika teuzi zake amekuwa akichagua wanawake katika kuongoza kwenye nafasi mbalimbali hivyo ni mama ambaye anatambua nafasi ya mwanamke katika uongozi, Sasa nimeona nikampe maua yake na zawadi mbalimbali kutoka Zanzibar na tunaungana na wenzetu ambao wanatokea katika mikoa mbalimbali ikiwemo Arusha,” amesema Khadija.
Nae dereva mwingine ambaye ataambatana katika msafara huo, Othuman Abdallah ‘Makombora’ amesema kutokana na kazi nzuri na mafanikio ambayo Raisi ameyafanya ameona ni vyema kuungana kwenda kumpongeza.
“Tunakwenda kujumuika kwenye sikukuu ya wapendanao na mama kwa sababu jitihada, mikakati na akiwa na lengo la kutaka kutufikisha Watanzania wote kwenye kilele Cha mafanikio na maisha bora, chanda chema huvikwa Pete hivyo tunakwenda kumpa mama maua yake,” amesema Makombora
#KonceptTvUpdates