Ofisa Mkuu wa Biashara wa Kampuni ya Simu ya Tigo, Shavkat Berdiev (kulia), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam leo kuhusu kampuni hiyo kudhamini Tamasha la Fiesta 2016. Kushoto ni Mwenyekiti wa Kamati ya Fiesta, Sebastian Maganga.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Prime Time Promotions, Joseph Kusaga, ambao ndiyo waandaaji wa tamasha hilo, akizungumza katika mkutano huo. Kutoka kulia ni Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Tanzania (Basata), Godfrey Mugereza, Ofisa Mkuu wa Biashara wa Kampuni ya Simu ya Tigo, Shavkat Berdiev na Mwenyekiti wa Kamati ya Fiesta, Sebastian Maganga.
Mwenyekiti wa Kamati ya Fiesta, Sebastian Maganga (kushoto), akizungumza katika mkutano huo.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Tanzania (Basata), Godfrey Mugereza (kulia), akichangia jambo kwenye mkutano huo.
Wanahabari wakichukua taarifa hiyo.
Mkutano ukiendelea. |
Na Dotto Mwaibale
TAMASHA la 15 la Fiesta mwaka 2016, linatarajiwa kuanza kutimua vumbi mwishoni mwa Agosti mwaka huu, likianzia jijini Mwanza.
Tamasha hilo ambalo linadhaminiwa na kampuni ya simu za mkononi, Tigo, linatarajiwa kuwa la aina yake kutokana na waandaji kufanya mabadiliko mbalimbali.
Akizungumza Dar es Salaam leo, Ofisa Mkuu wa Biashara wa Tigo, Shavkat Berdiev, alisema wameamua kuungana na waandaaji wa tamasha hilo kutokana na kutambua umuhimu wa sanaa kwa vijana.
Alisema kwamba, Tigo ni mtandao unaopendwa na wengi hasa vijana ndio maana wameamua kushirikiana nao katika tamasha hilo ambalo litakuwa la 15 tangu kuanzishwa kwake.
Mwenyekiti wa Kamati ya Fiesta, Sebastian Maganga, alisema kuwa, tamasha hilo linatarajiwa kuanza mwishoni mwa Agosti na kwamba litakwenda sambamba ya kuazimisha miaka 15 ya tamasha hilo.
“Tamasha hili litaanza rasmi mkoani Mwanza na kufuatiwa maeneo mengine ambayo ni pamoja na Kahama, Bukoba, Musoma, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Morogoro, Tanga, Kilimanjaro, Mtwara, Iringa, Mbeya na Dar es Salaam.
Alisema tamasha hilo watatumia kwa kujitathimini walichokifanya ambapo anaamini kama watafanikiwa kuendelea kuibua vipaji vingine kama ilivyokuwa kwa ‘Super Nyota Diva’ wa mwaka juzi ambaye anatamba kwenye muziki wa Bongo Fleva, Hellen George ‘Rubby’.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (Basata), Godfrey Mungereza, alisema kwamba, wao kama Baraza wametoa kibali kwa tamasha hilo, kwa sababu wamefata taratibu zote na wanatambua kwamba wanasaidia maendeleo ya sanaa nchini.
Tamasha hilo limeandaliwa na Kampuni ya Prime Time Promotions chini ya Mkurugenzi wake Mtendaji, Joseph Kusaga.